Azam na Yanga zafanya vizuri michuano ya Kimataifa

0
245

Jumamosi Agosti 24, Azam FC na Yanga zimetinga hatua ya kwanza ya michuano Afrika kwa ngazi ya vilabu baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo yao ya marudiano katika michuano ya kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa, Yanga ikiwa ugenini dhidi ya Township Rollers ya Botswana, imeibuka na ushindi wa bao moja kwa nunge lililofungwa na Juma Balinya kwa mkwaju wa adhabu ya nje ya eneo la hatari na kuwafanya wanajangwani hao kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao mawili kwa moja.

Azam FC wakiwa nyumbani wameinyuka Fasil Kenema ya nchini Ethiopia mabao matatu kwa moja kwenye mtanange uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex na kutinga hatua inayofuata kwa ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa mawili.

Azam FC imejipatia mabao yake kupitia kwa Richard Djoji aliyefunga mabao mawili katika dakika za 23 na 31 huku bao lingine likitiwa kimiani na Obrey Chirwa katika dakika ya 39, wakati Fasil Kenema wamepata bao la kufutia machozi kupitia kwa Mujib Kasim katika dakika ya 37.