Rais Magufuli ateta na Mabalozi

0
222

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali Duniani, wamempongeza Rais John Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.

Mabalozi hao 43 ambao wapo nchini tangu tarehe 13 mwezi huu, wametoa pongezi hizo walipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam



Wametoa pongezi hizo baada ya kutembelea mradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ikiwa ni pamoja na ule wa ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji, mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa unaoanzia Dar es salaam hadi Morogoro, jengo la Tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nojuma na mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es salaam.

Mabalozi hao wameeleza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii, umeleta heshima ya Tanzania katika Jumuiya ya Kimataifa.

Pia wamempongeza kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja, na wameahidi kuongoza vema katika mikutano ya Mabalozi wa SADC katika nchi wanazowakilisha kwa kuzingatia mwelekeo ambao Rais Magufuli ameutoa katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 17 na 18 mwezu huu jijini Dar es salaam.

Akizungumza baada ya kuwasilikiza Mabalozi hao, Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.

Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.