Rais Magufuli ataka ujenzi wa daraja ukamilike kwa wakati

0
2065

Rais Dkt. John Magufuli amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Hainan kutoka China kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa daraja la mto Sibiti ambalo linaunganisha mikoa ya Singida na Simiyu na kuondoa adha wanayopata wananchi hasa kipindi cha mvua.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa daraja la mto Sibiti baada ya kutoridhika na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.

Hadi sasa daraja hilo limechukua zaidi ya miaka sita kukamilika licha ya mkandarasi kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya gharama za ujenzi wa daraja hilo ambalo ujenzi wake unagharimu shilingi za kitanzania Bilioni 16.

Rais Magufuli pia amewaagiza watendaji wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano kumsimamia mkandarasi huyo ili akamilishe ujenzi huo kabla ya mwezi Machi mwakani na kama mkandarasi atashindwa kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa basi atachukua hatua zaidi dhidi ya wahusika akiwemo mkandarasi huyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi wamesema  daraja hilo ni mkombozi kwa wananchi wa mikoa ya Singida na Simiyu katika uimarishaji wa shughuli za kiuchumi kwenda ukanda huo.