Umoja wa Mataifa umeipongeza Tanzania kwa namna inavyotumia vizuri rasilimali zake za ndani, hali iliyoiwezesha kutekeleza miradi mbalimbali na kupunguza utegemezi kutoka nje.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dar es salaam na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, -Alvaro Rodriguez alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Rodriguez ambaye alikwenda kumuaga Waziri Mkuu amesema kuwa, Tanzania imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.
“Katika kipindi changu cha miaka mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania, nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na serikali, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa, pamoja na taasisi zake nchini”, amesema Rodriguez.
Katika hatua nyingine Rodriguez ameisifu Serikali ya Tanzania kwa namna ilivyoweza kuandaa na kuendesha vizuri mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika tarehe 17 na 18 mwezi huu.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa amemshukuru Mratibu Mkazi huyo wa Umoja wa Mataifa kwa pongezi alizozitoa, ambazo ni ishara kwamba anatambua jitihada zinazofanywa na serikali katika kutumia vizuri rasimali zake.
Awali, Waziri Mkuu Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini nchini Thamasanqa Dennis Mseleku ambaye alikwenda kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini.
Amempongeza Balozi Mseleku kwa ushirikiano na mchango alioutoa kwa Tanzania katika shughuli mbalimbali za maendeleo.