Rais John Magufuli ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri ya kuchunguza sampuli mbalimbali, kusimamia sheria za usimamizi wa kemikali na kudhibiti vinasaba vya binadamu.
Rais Magufuli ametoa pongezi hizo alipotembelea Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo jijini Dar es salaam.
Akiwa katika ofisi hiyo, Rais Magufuli amejionea namna mitambo ya uchunguzi ya kisasa inavyofanya kazi, ikiwemo kazi ya kuchunguza vinasaba vya miili ya watu waliofariki Dunia katika ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro Agosti 10 mwaka huu baada ya lori lililobeba mafuta kupinduka na kisha kulipuka moto.
Pia amejionea mitambo mipya ya uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, sumu, dawa za kulevya, kemikali na dawa inavyofanya kazi kwa haraka ambapo uchunguzi wa sampuli moja huchukua muda wa dakika 45 na unafanywa na vijana wa Kitanzania.
Akizungumza na Wafanyakazi wa Ofisi hiyo ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Rais Magufuli pia amewapongeza kwa uadilifu na uchapakazi wao katika majukumu mengine yakiwemo yale ya kutambua dawa za kulevya, kutoa ushahidi mahakamani na kufanya kazi katika mazingira yenye kemikali hatari kwa afya ya binadamu.
Amewaeleza Wafanyakazi hao kuwa, Serikali iliamua kuchukua hatua za kuiimarisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kununua vifaa vipya na vya kisasa, kuongeza wafanyakazi na kuibadili kutoka kuwa Wakala wa Serikali na kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wake na kuiongezea nguvu za kufanya kazi kwa uhuru zaidi ili kupata manufaa yanayotarajiwa.
“Nafahamu kuna wakati mlikuwa mnachunguza jambo na mnaandika ripoti ya uchunguzi wenu lakini hizo ripoti zilikuwa zinazimwa kwa sababu mlikuwa hamna nguvu, sasa mna nguvu nataka mfanye kazi”, amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, kutopokea rushwa, kutotoa siri na ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha watumishi wa ofisi hiyo wanaofanya uchunguzi wa masuala mazito wanakuwa salama na hawaingiliwi katika majukumu yao.
Amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo Profesa Ester Hellen Jason na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt Fidelice Mafumiko kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinazotumika kununua mahitaji mbalimbali vikiwemo vitenganishi vitumikavyo maabara.
Awali katika taarifa yake, Dkt Mafumiko aliishukuru Serikali kwa kutoa Shilingi Bilioni 5.338 kwa ajili ya kununulia mitambo na kuongeza wafanyakazi kutoka 110 hadi 294, hali iliyoongeza ufanisi wa kazi.
Ameongeza kuwa, kwa kipindi cha miaka Minne tangu mwaka 2015, vielelezo 204,974 vimechunguzwa, ambavyo ni sawa na wastani wa vielelezo 51,244 kwa mwaka, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 510 ikilinganishwa na rekodi za mwaka 2015/2016.