Watumishi wa sekta ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo – DRC wanaendelea kukabiliana na ugonjwa wa Surua ambao umezuka katika majimbo kadhaa.
Wizara ya Afya katika Jamhuri hiyo imesema kuwa majimbo 23 kati ya 26 yameathiriwa na ugonjwa huo wa Surua.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, zaidi ya watoto Elfu Mbili na Mia Saba wamefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa Surua kati ya mwezi Januari mwaka huu na mwezi huu wa Agosti, idadi ambayo ni kubwa kuliko ile ya wale waliofariki dunia baada ya kuugua ugonjwa Ebola katika kipindi chote cha mwaka 2018.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni Dola Milioni Mbili Nukta Tano tu kati ya Dola Milioni Nane Nukta Tisa za Kimarekani zilizokua zikihitajika kwa ajili ya kutekeleza mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo ndizo zimepatikana huko DRC.
Kwa upande wao Madaktari wa Kimataifa wasio na mipaka wamesema kuwa, ugonjwa wa Surua ndio unaoua watu wengi zaidi kuliko ugonjwa wa Ebola, ambao nao umeenea katika maeneo kadhaa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.