MARAIS WASTAAFU TANZANIA WAMKOSHA RAIS WA NAMIBIA DKT. HAGE GEINGOB

0
242
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa mara baada ya kuhutubia katika wa mkutano wa wa 39 wa Wakuu wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete na kulia ni Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi . PICHA NA IKULU

MWENYEKITI aliyemaliza muda wake katika Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye ni Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa kutokana ushirikiano na umoja wa viongozi wao.

Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi na serikali uliofanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam ,Dkt.Hage amesema; “Tanzania ni mfano wa kuigwa, ona marais wastaafu wamekaa pamoja na wameonesha ushirikiano mkubwa kwetu na hata mawaziri wastaafu wapo hapa, namwona John Malechela na wengine wengi kweli mnastahili pongezi” ameeleza Hage.

Aidha amempongeza Rais wa Kongo Felix Tshesekedi kwa kufanikisha kubadilishana madaraka kwa usalama nchini humo na kushauri kwa nchi jumuiya lazima zijikite katika kulinda amani na uhimilivu kama msingi mkuu wa maendeleo.

Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ndani ya ukanda huo Dkt.Hage amesema kuwa majanga ya mafuriko na vimbunga yamezikumba baadhi ya nchi za jumuiya hiyo zikiwemo Malawi na Msumbiji ambapo zaidi ya watu 3000 waliathirika.

“Shukrani za dhati ziende kwa nchi wanachama kwa kutoa msaada wa haraka kwa nchi zilizoathirika na majanga hayo na ninashauri tuchukue tahadhari za haraka ikiwa ni pamoja kuwashauri wananchi kupanda na kutokata miti na kutoa taarifa za haraka kwa wananchi kuhusiana mabadiliko ya tabia nchi,” ameeleza.

Pia amewahimiza nchi za Jumuiya kuwekeza zaidi katika kundi la vijana ili kuweza kupata maendeleo endelevu ili kufikia malengo ya mwaka 2025 waliyojiwekea kupitia programu mbalimbali zikiwemo za nishati, maji na miundombinu katika ngazi mbalimbali za kitaifa na kimataifa na hiyo ni pamoja na kuwa na kuangalia tafiti na gunduzi ili kuweza kuinua kundi hilo la vijana kupitia sera madhubuti. 

Alisema robo tatu ya wananchi wa Jumuiya hiyo ni vijana,hivyo wakitumika vizuri katika kuleta maendeleo nchi zetu zitapiga hatua kiuchumi.