KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dk.Stergomena Tax amezitaka nchi za jumuiya hiyo kuhakikisha mikakati yao ya kimaendeleo kwa kila nchi inauwiana na ile ya mikakati iliyowekwa na jumuiya hiyo.
Amesema changamoto kubwa iliyopo sasa ni kwamba kumekuwa na mikakati mizuri ya maendeleo kwa nchi za SADC lakini inakwama kutekelezeka kwasababu ya kutoendana na mikakati ya maendeleo ya nchi wanachama, hivyo ni vema kukawa na mikakati inayoendana.
Dk.Tax amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati uzinduzi wa Machapisho Matano yalioandaliwa na Kituo cha Utafiti na Machapisho Kusini mwa Afrika (SARDC) .Machapisho yaliozinduliwa la kwanza ni Mkakati wa SADC kuwajumuisha wanawake kwenye ulinzi na usalama ambalo limelenga kuwashirikisha wanawake katika eneo hilo la ulinzi na usalama.
Chapisho la pili linalozungumzia ufuatiliaji wa usawa wa kijinsia kwenye maendeleo alisema nchi nyingi za SADC bado zina hali mbaya wakati chapisho la tatu linazungumzia mkakati na mpango wa kushughulikia ukatili wa kijinsia, ufatiliaji wa maendeleo ya nishati na mpango mfupi wa kutathmini maendeleo ya miundombinu.
Akizungumzia zaidi wakati anaelezea machapisho hayo ,Dk.Tax amesema pamoja na uzuri wa machapisho hayo amesema kwa sasa kuna changamoto mbili kubwa ambazo zinazokwamisha utekelezaji wa mipango yao kwa nchi wanachama.
“SADC imekuwa ikiandaa mipango mingi mizuri kwa nchi wanachama lakini changamoto kubwa ni nchi kushindwa kutekeleza mikakati iliyopo. Changamioto hizo ni nchi wanachama kushindwa kuhuisha mipango ya SADC kwenye mipango ya kitaifa. Iwapo mipango haiwekwi kwenye mipango ya kitaifa ni vigumu utekelezaji kufanyika kwa wakati,”amesema Dk.Tax.
Pia amesema changamoto nyingine ni sekta binafsi kutoshiri kikamilifu kwenye ujenzi wa miundombinu na kuongeza kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na SARDC kati ya mipango 134 ambayo SADC walikubaliana utekelezaji ni asilimia 5 tu hali ambayo inatoa picha mbaya ya kufikia uchumi wa viwanda.
Hivyo ameshauri kwamba ni vema nchi za jumuiya hiyo pamoka na kuweka vipaumbele vyao, ni vema kukawa na mikakati ambayo inausiano na ile ya SADC ili kuhakikisha yote ambayo wanakubaliana yanatekelezwa na nchi wanachama.
Kuhusu machapisho hayo yaliyozinduliwa Mkurungezi Mkuu wa SARDC, Munetsi Madakufamba amesema kuwa machapisho hayo kwa sehemu kubwa yameonesha njia sahihi ya nchi wanachama wa SADC kufikia maendeleo jumuishi.
Amesema chapisho la kwanza la Mkakati wa SADC kuwajumuisha wanawake kwenye ulinzi na usalama na kufafanua kwa muda mrefu wanawake wa jumuiya hiyo wamekuwa wakiachwa nyuma na sasa umefika wakatu wa kuwashirikisha.
Akizungumzia chapisho la pili amesema limejikita katika ufuatiliaji wa usawa wa kijinsia katika maendeleo na kwamba chapisho hilo linaonesha bado nchi nyingi ziko kwenye hali mbaya, hivyo kuna kilasababu ya kuweka mikakati madhubuti. “Moja ya makubaliano ni kuwa na usawa wa kijinsia wa asilia 50 kwa 50 lakini ukweli uliopo bado nchi nyingi za jumuiya hiyo zimeshindwa kufikia lengo hilo.
“Katika eneo hili nchi ambazo zimefanya vizuri ni Afrika Kusini na Shelisheli ambapo uwakilishi upo 50/50 na kwa upande wa Tanzania nayo imejitajidi sana kwani imefikia asilimia huku asilimia 37.Hata hivyo amesema iwapo nchi zote wanachama zitashirikiana kwa pamoja kwa kuweka mikakati yao kwa mipango ya taifa ni dhahiri mafanikio yataonekana.
Wakati huo huo Mjumbe wa Bodi ya SARDC, Madaraka Nyerere amesema kwamba kituo hicho cha utafiti kimejikita katika kufanya tafiti katika ukanda huo kwa lengo la kusaidia sekretarieti ya SADC kufanya kazi zake za kuchochea maendeleo kwa usawa.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Tanzania imekuwa ikitekeleza makubaliano ya SADC hatua kwa hatua huku akilezea namna ambavyo Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mwanamke anapata nafasi na kupewa kipaumbele.
‘Serikali imekuwa ikitekeleza makubaliano hayo kwa kutoa mikopo kwa wakina mama ambapo zaidi Sh. bilioni 3 zimetolewa. Pia kuna ongezeko la ushiriki wanawake kwenye vikao vya maamuzi kutoka asilimia 22 mwaka 2010 hadi 37 kwa sasa.Pia uamuzi wa Serikali kutoa elimu bure umesaidia kuongeza idadi ya watoto wa kike kujiunga na elimu ya msingi na sekondari,”amesema.