WAJUMBE SADC WATEMBELEA VIWANDA 21, WAKOSHWA NA JUHUDI ZA SERIKALI

0
470
Mkurugenzi Mkuu wa Lodhia Group of Companies, Harminder Bhachu akiwaonesha Wajumbe wa mkutano wa 39 wa SADC nondo zikiwa tayari kusafirishwa maeneo mbalimbali kwa matumizi.

WAJUMBE wa Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC) wamepata  nafasi ya kutembelea viwanda 21 vinavyofanya uzalishaji kwa ajili ya kuangalia ubora wa bidhaa na mazingira ya uzalishaji kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Wakiwa katika viwanda hivyo wajumbe hao wamekiri na kuridhishwa na ambavyo Serikali ya Tanzania  ilivyodhamiria katika Uwekezaji katika viwanda huku wakieleza wazi Tanzania wanayo nafasi kubwa ya kumiliki soko la Jumuiya hiyo kwani kuna kila kitu zikiwemo malighafi za uhakika.

Mjumbe kutoka nchini Afrika Kusini wa Kampuni ya Flexion Renatus Joseph amesema kwamba yeye yupo katika sekta ya viwanda vya chuma jijini Johannesburg, Afrika Kusini na kwamba aliyoyashuhudia katika kiwanda cha Lodha Group of Companies yamenifanya abadili fikra zake kuhusu uwezo wa viwanda kwa nchi ya Tanzania.

Amesema amethibitisha kwa macho yake kuna matumizi makubwa ya teknolojia katika utengenezaji bidhaa za nondo na vifaa vingine vitokanavyo na chuma. “Hakika vikipatikana viwanda vingi vya namna hii SADC tutapiga hatua na tutakuwa na bidhaa zinazoleta ushindani ndani na nje ya Afrika,” amesema.

Wajumbe hao wakiwa kiwandani hapo yameelezwa kiwanda hicho cha chuma kilichopo Mkuranga mkoani Pwani ni miongoni mwa viwanda vilivyoitikia mwito wa Rais Dkt. John Magufuli kwa vitendo kuhusu Tanzania ya viwanda.

Akizungumza mbele ya ujumbe wa SADC waliotembelea kiwandani hapo Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhandisi Kamara Gombe amesema Tanzania kwa sasa inazalisha tani 200,000 za bidhaa za viwanda huku mahitaji ni tani 300,000.

“Hii maana yake kuna uhaba wa tani laki moja kwenye soko. Hivyo, Kampuni ya Lodhia ni miongoni mwa wadau wa viwanda wanaohakikisha Tanzania inajitegemea katika sekta ya viwanda.Hata hivyo, mbali ya uhitaji huo wa tani laki moja bado kuna tatizo la uhaba wa soko kwa kuwa wanazalisha tani 3000 kwa mwezi

“Lakini uwezo wao ni kuzalisha tani 10,000. Kazi yetu viwanda ni kulinda viwanda vya ndani, tutahakikisha tatizo hili tunalitafutia ufumbuzi ili hizi tani 7,000 zilizobaki ziweze kuzalishwa,” amesema Gombe.

Wakati Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Toni Filbert amesema wilaya hiyo pamoja na Mkoa wa Pwani kwa ujumla wanazo fursa nyingi za uwekezaji kutokana na ardhi kubwa yenye rutuba. Vilevile, kuna bidhaa nyingi za kimkakati zinazozalishwa na wazawa.

Akitoa maelezo kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Lodhia Group of Companies, Harminder Bhachu alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1996 wakiwa wanafanya biashara ya jumla ya kuuza vyuma ambapo mwaka 2004 ndio walianza kuzalisha vyuma katika kiwanda kilichopo mkoani Arusha.

“Vilevile tuligeukia bidhaa nyingine ikiwemo mabomba ya maji, Gypsum Board, mapipa ya kuhifadhia maji na bidhaa nyingine za ujenzi kwa kuhakikisha Tanzania inajitosheleza katika vifaa vya ujenzi bila kuagiza nje ya nchi,” amesema Bhachu na kufafanua wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuwahamasisha kuwekeza kwa nguvu na pia amesaidia kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa kila kampuni bila kupendelea.

Hata hivyo katika ziara hiyo, wajumbe wa SADC pia walipata fursa kutembelea kiwanda cha kusindika matunda cha Bakhresa Group of Companies kilichopo Mwandege Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Wajumbe walivutiwa na namna ya kipekee waliyoonyesha wafanyakazi wa kiwanda hicho katika usindikaji matunda, mitambo ya kisasa na usafi wa hali ya juu pia ulionyesha ni namna gani kampuni hiyo ilivyo tayari kuliteka soko la SADC.