Wizara ya afya yaeleza inavyowahudumia majeruhi ajali lori la mafuta- Morogoro

0
574

Wizara ya afya yaeleza inavyowahudumia majeruhi ajali lori la mafuta Morogoro – Mwananchi

Wizara ya Afya nchini Tanzania imeeleza taratibu mbalimbali zinazofanywa kuhakikisha majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro wanapata matibabu stahiki.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Agosti 10, 2019 na waziri wa wizara hiyo,  Ummy Mwalimu alipokuwa akielezea huduma mbalimbali za dharura zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro alipo majeruhi wa ajali hiyo.

Ajali hiyo imetokea leo baada ya lori la mafuta ya petroli kupinduka eneo la Msamvu na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta hayo.

“Tumepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya moto iliyotokea leo Morogoro, Serikali kupitia wizara ya afya tupo kazini tayari Bohari ya Dawa (MSD) wapo njiani kupeleka dawa, vifaa na vifaa tiba vinavyohitajika haraka kwa magonjwa ya moto.”

“MSD wanapeleka vifaa tiba kama vile fluids, strong analgesics, Tetanus toxoid, burn creams, bed credos, gauzes, giving sets, urine bags, catheters  kwa ajili ya kuhudumia majeruhi,” amesema Ummy.

Amebainisha kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Zainab Chaula, mganga mkuu wa Serikali na timu ya wataalam kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wapo njiani kuelekea Morogoro ili kuongeza nguvu ya kuhudumia majeruhi.