TFS yajidhatiti kuhifadhi Misitu na kutoa Elimu ya Ufugaji Nyuki

0
270
Meneja Masoko wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Mariam Kobero akizungumza na wanahabari katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya nne ya viwanda kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo washiriki mbalimbali wamekuwa wakifika kupata maelezo kuhusu wakala hao wanavyofanya shughuli zao na wengi wao wamevutiwa zaidi na utalii wa misitu na ufugaji wa nyuki wenye tija kibiashara.

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imesema kupitia Maonesho ya nne ya viwanda kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imepata nafasi ya kueleza fursa mbalimbali zinazopatikana huku wakitumia nafasi hiyo kutangaza utalii unatokana na uhifadhi za misitu asilia.

TFS ambayo imeweka banda lake kwenye maonesho hayo yanayoendelea katika Ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalim Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo washiriki mbalimbali wamekuwa wakifika kupata maelezo kuhusu wakala hao wanavyofanya shughuli zao na wengi wao wamevutiwa zaidi na utalii wa misitu na ufugaji wa nyuki wenye tija kibiashara.

Meneja Masoko wa TFS Mariam Kobero amewaambia waandishi wa habari waliofika katika banda lao lililipo kwenye maonesho hayo kuwa kupitia maonesho hayo washiriki kutoka nchi mbalimbali wamekuwa wakielimishwa namna TFS inavyotekeleza majukumu yake kwa niaba ya Serikali na hasa ya uhifadhi wa misitu asilia na ufugaji nyuki na mazao yake.

“Tumekuwa tukitoa elimu kuhusu TFS na majukumu yake.Hata hivyo sehemu ya washiriki wameonekana kutaka kufahamu zaidi kuhusu ufugaji nyuki kibiashara, wengine wameeleza wanavyovutiwa na ubora wa asali ya Tanzania na ukweli ni kwamba mazao ya nyuki yameendelea kuwa na mahitaji ya kila siku.


Meneja Masoko wa TFS Mariam Kobero akisistiza jambo kwa waandishi wa habari hawapo pichani kuhusiana na huduma za wakala hiyo.

“Hata hivyo katika eneo la asali pamoja na mambo mengine tumekuwa tukieleza kuwa ili kuhifadhi vizuri asali kwenye chupa aihitaji kuwa na mtambo mkubwa bali unaweza kuwa na mtambo mdogo na asali ikahiwekwa vizuri kabisa.Tumekuja na mtambo mdogo sana ambao unatumika kujaza asali,wengi wamevutiwa nao,”amesema Kobero.

Ameongeza katika mazao ya nyuki mbali ya asali, inapatikana nta, ambayo inatumika kutengeza mishumaa, pia inatumika kutengeneza vilainishi vya midomo na mafuta ya kulainisha ngozi.Hivyo watakaojikita kwenye ufugaji nyuki na mazao yake kuna faida nyingi ambazo wanaweza kuzipata.

Pia amesema banda lao limekuwa na mvuto kwasababu watu wengi hawafahamu kama serikali inafuga nyuki kupitia TFS huku akifafanua kuwa ni wakati muafaka kwa nchi za SADC kununua asali ya nchini Tanzania kwani ni bora na ladha yake ni tofauti na asali nyingine.

Kuhusu utalii wa unaotokana na uhifadhi wa misitu asilia , Kobero amesema TFS imeona haja ya kutumia nafasi hiyo kuelezea aina hiyo ya utalii kwa nchi za SADC na lengo ni kuwaambia kuwa Tanzania kuna utalii ikolojia, hivyo ni vema wakafika kwenye misitu iliyopo nchini ambapo kwa sasa kuna misitu asilia 17.

“Utalii ikolojia ni eneo zuri kwa utalii, hivyo tunazihamasisha nchi za SADC kuja kuwekeza kwenye utalii huo na wakati huo huo tunawahamasisha wafike kwenye vivutio hivyo ambavyo kwa anayefika atapenda kwani mazingira ya misitu yetu ni tulivu na ndani yake kuna utalii wa kila aina,amesema Kobero.

“Tulichobaini utalii wa misitu kwa nchi za SADC una nafasi kubwa  na kuna fursa nyingi za kibiashara na kiuwekezaji.Tunafahamu kwa nchi nyingi za SADC utalii wa ikolojia ni mpya na bahati nzuri kwenye utalii huu nchi yetu iko vizuri.Washiriki wengi wameahidi kutembelea misitu ya asili,”amesema Kobero.