TPDC YAZIHAKIKISHIA NCHI ZA SADC TANZANIA KUNA GESI YA KUTOSHA

0
262
Baadhi ya washiriki wa majadiliano yaliyojikita kuzungumzia umuhimu wa mafuta na ujenzi wa miundombinu katika kuondoa umasikini kwa nchi za Jumuiya za maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) ambapo Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania(TPDC),wametumia nafasi hiyo kutoa uzoefu wao

SHIRIKA la Maendeleo la Petroli Tanzania(TPDC) limezihakikisha nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) kuwa wana gesi ya kutosha na wanajivunia kuwa na uzoefu wa miaka 50 katika ujenzi wa miundombinu ya gesi na mafuta.

Pia limesema kwa sasa mahitaji ya gesi yanaongezeka na tayari wameanza kufanya mazungumzo na nchi tano za Kenya, Zambia, Uganda , Malawi na DRC ili wapelekewe gesi kwenye nchi zao.


Mmoja wa washiriki akifutulia mjadala kuhusu gesi na mafuta katika kuondoa umasikini kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TPDC James Mataragio wakati anazungumza na waandishi waliokuwa kwenye mjadala ambao mada yake ilijikita kuzungumzia mafuta na ujenzi wa miundombinu katika kuondoa umasikini.

Hivyo wametumia nafasi hiyo kueleza kuwa mahitaji ya gesi kwa nchi mbalimbali za SADC ni makubwa na ndio maana kuna nchi wanaendelea kuzungumza nazo ili kuhakikisha nishati ya gesi inawafikia.

“Kuhusu nafasi ya soko ya gesi, mahitaji ni makubwa na yanaongezeka kila siku .Nchi za Kenya, Zambia, Uganda , Malawi na DRC wameomba kusambaziwa gesi.

“Hivyo kuna uwezekano wa kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa, kujenga bomba la gesi kutoka Tanga kwenda Uganda na tayari kuna uwezekano wa kutumia mkuza wa kupitisha mafuta mazito kwenda Ndola Zambia ambalo litatumika kupitisha gesi,”amesema Mataragio.

Alipoulizwa kuhusu nafasi ya TPDC ,Mataragio amejibu wao wamekuwa na uzoefu mkuwa katika eneo la mafuta na gesi na wamekuwa wakifanya tafiti nyingi katika eneo hilo ikiwemo kugundua mafuta na gesi.

“Tanzania tunao uzoefu kwa miaka 50 katika ujenzi wa miundombinu na hasa kwenye gesi na mafuta. Kuna mabonda kama nne ambayo tumewahi kujenga.Tumejenga bomba kutoka Tanzania kwenda Zambia ambalo linasafarisha mafuta mazito.

“Tumejenga bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa ajili kusafirisha gesi, bomba la Msimbati hadi Mtwara na bomba la kutoka Songo songo kwenda Dar es Salaam,”amesema.

Hivyo amesema wao wametumia majadiliano hayo kuelezea uzoefu wao katika kujenga miundombinu hiyo pamoja na kuisimamia na kwa sasa kuna ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kuja Tanzania.