Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika –SADC Dkt Stragomena Tax amesema Miradi mkubwa inayotekelezwa na Tanzania itasaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa viwanda katika ukanda huo.
Akihutubia wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 4 ya viwanda ya Jumuiya ya SADC Dkt Tax amesema, umeme utakaozalishwa kwenye mradi wa kuzalisha umeme wa bonde la mto Rufiji utasaidia na nchi nyingine za jirani na Tanzania.
Dkt Tax amesema, mradi huo umekuja wakati muafaka kwani kwenye SADC kwa sasa msisitizo umewekwa kwenye ukuaji wa viwanda na kwa kiasi kikubwa viwanda vinategemea umeme.
Kuhusu ujenzi wa reli ya Kisasa ya Standard Gage Dkt Tax amesema, huo ni mradi mkubwa utakaorahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo katika nchi hizo kwenda kwenye maeneo mengine.
Hata hivyo ameisifu serikali ya awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Dkt John Magufuli kwa hatua anazochukua za kuboresha bandari zake na kusema hiyo itarahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa katika nchi za SADC kwenda maeneo mengine ulimwenguni.
Story by. James Range