Serikali imesema itatumia kamati mbalimbali za Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuwasaidia wabunifu katika sayansi na teknolojia ili wafanye utafiti wenye kutatua changamoto za jamii.
Akizungumza katika maonesho ya tisa ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema kupitia kamati ya mawaziri wa sayansi, teknolojia na ubunifu, wamejiwekea mipango ya kuendeleza wabunifu.
Waziri Ndalichako amesema suala la kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu limepewa kipaumbele.
“Kwa sasa tumeweka mipango na taratibu za kuwatambua wanasayansi na wabunifu ambapo jumuiya hii inaingia katika mapinduzi ya viwanda, hivyo wabunifu ni watu muhimu,” amesema.
Profesa Ndalichako amesema maonyesho hayo yana ashiria kuwa elimu inayotolewa inakidhi na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za jamii.
“Najivunia kuona kuwa idadi ya wasichana imezidi kuongezeka ambapo kwa mwaka huu wasichana ni 88 sawa na asilimia 46, ya washiriki wote katika maonesho hayo” alisema Profesa Ndalichako.
“Hata tafiti zilizofanyika kwa mwaka huu zimekuwa na kiwango bora na zenye kulenga kutatua changamoto zilizopo katika jamii,” amesema Profesa Ndalichako.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nundu, amesema kwa muda mfupi vijana kupitia YST wamefanya utafiti unaoonyesha kutatua changamoto za jamii.
“Mfumo huu ni mzuri kwa kuwa umeweza kujenga vijana wadogo wenye uwezo wa kufanya tafiti zenye weledi zinazosaidia kuchangia ukuaji wa taifa,” amesema Dk. Nundu.