Rais Magufuli awataka watanzania kutembea kifua mbele

0
347

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watanzania Kujiamini na kuamua kutekeleza miradi mbalimbali ya nchi kwa kutumia kodi zao

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la tatu la Abiria katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Jijini Dar es salaam.

Akihutubia Mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es salaam waliojitokeza katika Hafla hiyo, Rais Magufuli amewataka watanzania kutembea kifua mbele wakati wote kwani miradi mingi mikubwa inajengwa kwa fedha za ndani.

Akizungumzia Mradi wa jengo hilo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka, Rais Magufuli amesema, utasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini.

Rais Magufuli amesema, kwa kutambua umuhimu wa usafiri wa Anga kama kichocheo cha ukuaji wa sekta mbalimbali, serikali inaendelea kuchukua hatua zinazolenga kuimarisha sekta ya usafiri wa Anga ikiwa ni pamoja na kuongeza ndege tatu nyingine na hivyo Tanzania kutarajiwa kuwa na ndege 11.