Rais wa Tanzania, John Magufuli ametengua uteuzi wa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini (DED) nchini Tanzania, Kayombe Rioba kutokana na utendaji usioridhisha wa usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Agosti 1, 2019, jijini Dar es Salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo amesema Rioba ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Waziri Jafo amebainisha baadhi ya kasoro ambazo mkurugenzi huyo ameshindwa kusimamia ni ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo Rioba alinunua dawa ya kupulizia mchwa katika majengo Sh66 milioni ambazo ni zaidi ya matarajio ya matumizi ya fedha ya eneo hilo.
Amesema mkurugenzi huyo ameshindwa kufuatilia taratibu za manunuzi na miongozo yote ya matumizi ya fedha na manunuzi yalikuwa zaidi ya Sh145 milioni na kupotea kwa Sh42 milioni.
Kutokana na uamuzi huo, Waziri Jafo amesema Godfrey Mlowe ambaye meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) Morogoro vijijini kukaimu nafasi hiyo ambapo atapaswa kusimamia miradi na mambo yote katika halmashauri hiyo ikiwemo kukamilisha ujenzi hospitali hiyo ya wilaya pamoja na kuanza ujenzi wa vituo vya afya vya Mikese na Kinoko vilivyopelekewa fedha hivi karibuni.