Askari 10 Sudan Kusini wahukumiwa kifungo jela

0
2211

Mahakama ya Kijeshi ya Sudan Kusini imewahukumu kifungo cha kati ya miaka Saba na maisha jela, askari kumi wa nchi hiyo baada ya kupatikana na makosa ya kuwadhalilisha wafanyakazi wa kigeni wa kutoa msaada pamoja na mauaji ya mwandishi wa habari wa nchi hiyo.

Habari kutoka Sudan Kusini zinasema kuwa, askari hao walitenda makosa hayo mwaka 2016 baada ya kuvamia hoteli ya Terrain iliyopo katika mji wa Juba, ambapo wafanyakazi hao watano walidhalilishwa.

Mahakama hiyo pia imeagiza kulipwa fidia ya dola elfu nne za Kimarekani kwa kila muathirika wa tukio hilo na kuiagiza serikali kumlipa mmiliki wa hoteli hiyo Mike Woodward ambaye ni raia wa Uingereza zaidi ya dola milioni mbili za Kimarekani.

Wanadiplomasia mbalimbali pamoja na wafanyakazi kadhaa wa kutoa msaada walifika katika mahakama hiyo ya Kijeshi ya Sudan Kusini kusikiliza hukumu ya kesi hiyo.