Rais John Magufuli ameagiza kuchukuliwa hatua watu wote waliohusika kukwamisha kukamilika kwa mradi wa maji katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya Wakazi wa wilaya hiyo kumueleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kukosekana kwa maji safi na salama huku wilaya hiyo ikiwa na mradi mkubwa wa maji ambao haujawafaidisha.
Amesema kuwa serikali haiwezi kuvumilia kuona mkandarasi aliyekua akitekeleza mradi huo kushindwa kuukamilisha kwa muda wa miaka Minane wakati amekwishalipwa fedha.
Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa pamoja na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Bunda ndani ya kipindi cha wiki moja ili kubaini chanzo cha kukwama kwa mradi huo.
Rais Magufuli amewahakikishia wakazi hao wa Bunda kuwa ni lazima watapata maji saji na salama kupitia mradi huo kwa kuwa suala hilo atalishughulikia yeye mwenyewe.