Boris Johnson kuwa Waziri Mkuu mpya Uingereza

0
257

Meya wa zamani wa jiji la LONDON BORIS JOHNSON anatarajiwa kushika madaraka ya uwaziri mkuu wa Uingereza  baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha  CONSERVATIVE nchini humo.

BORIS JONSON ambaye pia amewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, ameibuka mshindi wa nafasi ya  uongozi katika chama hicho kwa kupata kura 92,153 dhidi ya mpinzani wake JEREMY HUNT, ambaye ni waziri wa sasa wa mambo ya nje wa Uingereza aliyepata kura 46,656.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa  mshindi,kiongozi huyo amesema atahakikisha anashirikiana na viongozi wenzake ili kufanikisha mpango wa Uingereza kujitoa katika umoja wa Ulaya ifikapo OKTOBA 31, Mwaka huu.

Pia amemshukuru mtangulizi wake TERESA MAY kwa kufanya kazi pamoja juu ya mpango licha ya kuwa  alijiuzulu kwa kushindwa kulishawishi bunge la Uingereza  kuhusu mpango huo wa kujitoa katika umoja wa ULAYA EU.

Tayari salamu za pongezi kwa ushindi wake zimeanza kutolewa na viongozi mbalimbali Duniani, akiwemo Rais DONALD TRUMP wa Marekani aliyesema ana imani na BORIS JONSON katika kuiongoza serikali ya Uingereza.

Uchaguzi wa uongozi katika chama cha CONSERVATIVE huko Uingereza umefanyika baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa kiongozi wa chama hicho THERESA MAY baada ya kushindwa kufanikisha mpango wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa ULAYA.