Rais Magufuli akutana na Mzee Msekwa

0
2261

Rais John Magufuli amekutana na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Pius Msekwa na Mkewe Mama Anna Abdallah katika Ikulu Ndogo ya Nansio – Ukerewe mkoani Mwanza.

Baada ya mazungumzo yao, Mzee Msekwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kufanya ziara yake ya kwanza katika kisiwa cha Ukerewe tangu achaguliwe kuwa Rais, na kwa serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kisiwani humo ikiwa ni pamoja na ile ya maji, ujenzi wa barabara na ununuzi wa meli mpya katika ziwa Viktoria.

Mzee Msekwa pia amezungumzia utendaji kazi wa Rais Magufuli na serikali ya awamu ya Tano, ambapo amesema kuwa mageuzi makubwa yanayofanywa yanaandika historia kama alivyofanya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Kwa Nyerere tulisema kama sio juhudi zako Nyerere, maendeleo tungepata wapi, na huyu Rais Magufuli naye tutasema kama sio juhudi zako meli, Dreamliner, reli na mengine mengi tungepata wapi?” amesisitiza Mzee Msekwa.

Kwa upande wake Mama Anna Abdallah ambaye ni Waziri Mstaafu amemshukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi na kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi na ametoa wito kwa wanawake wote waliopata nafasi za uongozi kuonesha mfano mzuri kwa kuchapa kazi kwa juhudi, uadilifu mkubwa na kujiamini ili wengine wengi zaidi waendelee kupata nafasi.

“Nafurahishwa sana na kazi zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli, kwa hakika anatutendea mazuri mengi sana sisi Watanzania na sisi wanawake” amesema Mama Anna Abdallah.

Rais Magufuli amekutana na Mzee Msekwa na Mama Anna Abdallah kando ya ziara yake katika kanda ya ziwa ambayo inaendelea mkoani Mara.