WHO yasaidia DRC kukabiliana na Ebola

0
439

Wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo – DRC imeelezea kufurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Shirika la Afya Dunia – WHO ya kutangaza kuwa kuna umuhimu wa kuchukua hatua za dharula Kimataifa za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri hiyo.

Waziri wa Afya wa DRC, – Oly Illunga amesema kuwa, hatua hiyo ya WHO itawasaidia Wataalam wa afya wa Jamhuri hiyo, kukabiliana na ugonjwa huo, kazi ambayo wamekua wakiifanya kwa zaidi ya mwaka mmoja hivi sasa.

Katika mkutano wake uliofanyika huko Geneva, – Uswiss, WHO ilifikia hatua ya kutangaza kuchukuliwa hatua za dharula Kimataifa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya kugundulika kwa mgonjwa mmoja katika mji wa Goma, mji uliopo katika eneo la Mashariki.

Kwa mujibu wa wizara ya Afya ya DRC, maafisa wa afya katika mji huo wa Goma unaokaliwa na zaidi ya watu Milioni Moja, wamejiweka tayari kukabiliana na ugonjwa huo.

Mtendaji Mkuu wa WHO, – Tedros Adhanom amesema kuwa kutokana na hali ya ugonjwa wa Ebola ilivyo sasa huko DRC, zinahitajika jitihada za Kimataifa katika kukabiliana na ugonjwa huo.