Nyota wa Taifa stars wanaocheza nje wawasili nchini

0
2153

Nyota wanne wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa stars) wanaocheza soka nje ya nchi wamewasili nchini na kuanza kufanya mazoezi na wenzao tayari kwa mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa mwishoni mwa juma nchini Uganda.

Nyota hao ni nahodha Mbwana Samatta, Ramadhan Kessy, Rashid Mandawa na Thomas Ulimwengu.

Nyota wengine waliotarajiwa kuwasili ni mlinzi Abdi Banda, Simon Msuva, Shabaan Idd Chilunda, Farid Mussa na nahodha msaidizi Himid Mau.

Kikosi hicho cha kocha Emmanuel Amonike kilianza mazoezi wiki moja iliyopita kwa ajili ya kujianda na mchezo huo wa kufuzu kwa mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda ambapo wachezaji alioanza nao mazoezi walikuwa wanacheza soka hapa nyumbani.

Huo ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars baada ya kutoka sare katika mchezo wa kwanza dhidi ya Lesotho mwaka mmoja uliopita na hivyo wanahitaji kushinda ili kuweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.