Waziri Biteko:Wafanyabiashara Wasitoroshe Madini Watumie Masoko ya Madini Tanzania

0
239

Waziri wa Madini Dotto Biteko amewataka wafanyabiashara wa madini nchini kutumia masoko ya madini yaliyofunguliwa na serikali badala ya kujihusisha na utoroshaji wa madini unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu huku akitolea mfano kwa watu watatu wanaodaiwa kutorosha madini mkoani Arusha  yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 958 kwa lengo la kupeleka nchi jirani.

Waziri Biteko ametoa kauli hiyo jijini Arusha mara baada yakuona hali halisi ya madini yaliyotoroshwa pamoja na shehena nyingine ya madini yaliyohifadhiwa katika baadhi ya nyumba za watuhumiwa,amesema ni kinyume cha sheria ya madini kuhifadhi madini majumbani pasipo  na kibali.

Shehena ya madini ikiwa uani nyumbani kwa mmoja wa wakazi wa jijini Arusha.

Shehena hii imebainika baada ya polisi jijini Arusha kuwakamata watu wawili wakitorosha madini kwa kutumia usafiri wa basi kwenda nchi jirani ambao wametaja maficho yao. 

Msako huu umeongozwa na Waziri wa Madini Doto Biteko, mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, Kamanda wa Polisi Jonathana Shana na wataalam wa madini.

Akizungumzia tukio hili Waziri Biteko amemekemea tabia hii na kusema iwe fundisho kwa Watanzania wanaojihusisha na utoroshaji wa madini na akawataka wafanyabiashara kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa na serikali.

Aidha Waziri Biteko amesema yapo baadhi ya masoko ya madini ambayo hayafanyi vizuri ikiwemo Katavi ambapo ametuma timu ya wataalamu wa madini kubaini tatizo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa Mrisho Gambo, ameomba mahakama kutoa adhabu kali kwa wanaobainika kujihusisha na utoroshaji madini.

Kufuatia kiasi cha kilo 31.5 kukamatwa mkoani Arusha, Gavana Mkazi wa Benki Kuu Tawi la Arusha, Charles Yamo, amesema wamepokea madini hayo na yatahifadhiwa kwa mujibu wa sheria huku Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana akisema wamejipanga kuhakikisha madini hayatoroshwi.