Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amewahakikishia wananchi wote kuwa nchi iko salama na kuwataka kuendelea nashughuli zao za kila siku kama kawaida.
Akitoa ufafanuzi kuhusu hali ya usalama hapa nchini Waziri Lugola amesema serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usalama iko imara kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu.
Siku moja baada ya Ubalozi wa Marekani hapa nchini kutoa taarifa ya tahadhari kuhusu tetesi za uwezekano wa kufanyika kwa mashambulio katika baadhi ya migahawa na hoteli zinazotembelewa na watalii katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam na kuwaonya raia wa taifa hilo kuchukua tahadhari serikali na jeshi la polisi limewatoa hofu wananchi kwa kusema hali ni shwari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amesema serikali kwa kushirikiana na vyombo vya usalama iko imara kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro amesema hakuna tishio lolote la kigaidi nchini na kwamba jeshi la Polisi lipo imara kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na kuwataka wananchi kuendelea kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kujenga uchumi wa nchi.
IGP Sirro amewataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa faida na si kuwajengea hofu wananchi.
Halikadhalika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imemwita Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini kahoji kuhusu taarifa iliyotolewa na Ubalozi huo ambapo mwakilishi wa Kaimu Balozi huyo Ann Marie Warmenhoven – Tilias amekiri kuwa Ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee wakitambua kuwa Ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Mnyepe amewataka wananchi, Jumuiya za Kimataifa na wageni waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini.
