Ubadhirifu Kampuni ya Huduma za Meli wamkera Rais

0
2438

Rais John Magufuli ameeleza kukerwa na ubadhirifu uliokua ukifanyika katika Kampuni ya Huduma za Meli nchini.

Amesema kuwa ubadhirifu huo umesababisha kampuni hiyo kushindwa kujiendesha ikiwa ni pamoja na kutolipa mishahara ya wafanyakazi kwa muda wa miezi 27 ambayo ni takribani Shilingi Bilioni 3. 7.

Rais Magufuli ameahidi kuwa serikali itatoa pesa hizo ambazo watalipwa wafanyakazi hao ndani ya kipindi cha wiki Mbili.

Ameyasema hayo mara baada kushuhudia hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa meli mpya, chelezo na ukarabati wa meli ya MV Viktoria na MV Butiama katika ziwa Viktoria.

Hata hivyo Rais Magufuli amempongeza Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo ya Huduma za Meli nchini Erick Hamisi ambaye ameonyesha muelekeo mzuri wa kuiendeleza kampuni hiyo na kumuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kumpatia nafasi ya Meneja Mkuu na si Kukaimu nafasi hiyo.

Amesisitiza kuwa azma ya serikali ya awamu ya awamu ya Tano ni kuwekeza katika miundombinu mbalimbali yenye manufaa kwa Watanzania wote.

Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kulipa kodi ili serikali iweze kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.