Wydad walalamikia mchezo wake na Esperance

0
548

Rais wa timu ya Wydad Casablanca ya Morocco, – Said Naciri amelitaka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kufanya uchunguzi wa kina ili kupata jibu la  nini kilitokea hadi kuvurugika kwa mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baina ya timu hiyo na timu ya Esperance ya nchini Tunisia.

Katika mchezo huo,  wachezaji wa Wydad waligoma kuendelea na mchezo  baada ya goli lao la kusawazisha kukataliwa na muamuzi na mashine maalumu ya VAR kushindwa kutoa maamuzi kwa taarifa, na  hivyo Esperance wakapewa ushindi na kutunukiwa ubingwa.

Rais huyo wa Wydad Casablanca amesema kuwa  timu yake ni waathirika wa wa tukio hilo, hivyo lazima CAF wafanye uchunguzi wa kina ili kuweza kuliokoa soka la Afrika kwa kuwa tukio hilo limeharibu taswira nzima ya soka hilo.

Mapema, Muamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Gambia baada ya kulikata goli lililofungwa na Walid Karti kwa kisingizio mfungaji alikuwa ameotea, Muamuzi huo alikata kwenda kuangalia mashine ya VAR hadi alipolazimishwa na wachezaji wa Wydad Casablana kwenye dakika ya 59 na alipoenda akaambiwa mashine hiyo ni mbovu.

Kamati ya Utendaji ya CAF inatarajiwa kukutana hapo kesho kwa lengo la kujadili suala hilo, huku Chama Cha Soka cha Morocco kikisema kuwa kinaiunga mkono timu hiyo ya Wydad Casablanca na kitaisaidia ili iweze kupata haki yake.