Mgomo waathiri usafiri wa anga Sudan

0
275

Mgomo wa nchi nzima ulioitishwa na vikundi vya waandamanaji nchini Sudan,  kwa lengo la kushinikiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini humo, umeathiri usafiri wa anga wa nchi hiyo.

Habari zaidi kutoka nchini Sudan zinasema kuwa, kampuni nyingi za ndege nchini humo zimefuta safari zake za ndege na hivyo kuathiri shughuli zote za usafirishaji kwa njia ya anga.

Taarifa zilizotolewa na mashirika mengi ya ndege ya nchi ya Sudan zimesema kuwa,  hayawezi kuendelea na safari kwa kuwa ndege haziwezi kupaa wala kutua katika viwanja vya ndege,  kwa kuwa wafanyakazi wa viwanja hivyo wanashiriki katika mgomo huo.

Raia wa Sudan wameapa kuendelea na mgomo pamoja na maandamano hayo, yenye lengo la kulishinikiza Jeshi la nchi hiyo kurejesha utawala wa kiraia.

Jeshi la Sudan lilichukua jukumu la kuongoza serikali ya mpito ya nchi hiyo,  baada ya kufanyika mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Omar Al-Bashir,  aliyeiongoza Sudan kwa takribani miaka Thelathini.