Bobi Wine azuiliwa kwenda nje ya nchi

0
2615

Mbunge wa upinzani nchini Uganda ambaye pia ni Mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anayedaiwa kupigwa na kuteswa baada ya kukamatwa mapema mwezi huu, amezuiliwa kuondoka nchini humo kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi.

Mwanasheria wa mbunge huyo Robert Amsterdam amedai kuwa mteja wake Bobi Wine amezuiliwa kuingia katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Uganda na badala yake amechukuliwa na polisi ambao wanadaiwa kumpeleka katika hospitali ya serikali.

Amsterdam amesisitiza kuwa kipaumbele cha Bobi Wine kwa sasa ni kupata matibabu nje ya nchi na si kutoroka nchini humo.

Kabla ya kuzuiliwa kwa Bobi Wine katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Uganda, mbunge mwingine wa upinzani Francis Zake pia alizuiliwa kwenye uwanja huo kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi.

Bobi Wine anakabiliwa na makosa ya uhaini, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mawe gari la Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni na aliachiliwa siku ya Jumatatu kwa dhamana kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa huku ikielezwa kuwa yuko katika hali mbaya.