Venus na Serena Williams kukutana US OPEN

0
2800

Ikiwa ni miaka Ishirini imepita tangu walipokutana kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kuwania taji kubwa la tenisi duniani (Grandslum), wanadada ndugu Venus na Serena Williams watakutana katika hatua ya 16 bora ya mashindano makubwa ya tenisi ya wazi ya Marekani (US OPEN) baada ya kushinda michezo yao ya hatua ya tatu.

Mchezo huo unachezwa usiku wa kuamkia Septemba Mosi mwaka huu kwenye dimba la Arthur Ashe na itakuwa ni mara ya 30 kwa wanadada hao ndugu kukutana ambapo kwa mara ya mwisho walikutana katika mashindano ya Indian Wells mwezi Machi mwaka huu na Venus kuibuka mshindi.

Akizungumzia mchezo huo Venus ambaye ni mkubwa kwa Serena kwa tofauti ya miaka Miwili amesema kuwa angalau kutakuwa na usawa katika mchezo huo akirejea fainali ya mashindano ya wazi ya Australia walipokutana mapema mwaka 2017 ambapo Serena alikuwa na ujauzito wa mwanaye wa kike aitwaye Olympia.

Miongoni mwa michezo yao ya kukumbukwa ni pamoja na ule wa mwaka 1998 katika mashindano ya wazi ya Australia kwenye hatua ya pili ambapo Venus alikua na umri wa miaka 17 huku akishika nafasi ya 16 kwenye viwango vya ubora, aliibuka na ushindi wa seti mbili kwa bila za 7-6 na 6-1 dhidi ya mdogo wake Serena ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15 na alikua katika nafasi ya 53 kwenye viwango vya ubora.

Mwaka 2003 kwenye fainali za Australian Open, Serena alishinda taji lake la kwanza la mashindano hayo na kuwa mwanamke wa kwanza baada ya Steffi Graf mwaka 1994 kushinda mataji manne ya Grandslum ndani ya mwaka mmoja lakini ukawa mchezo wa nne kwa dada yake Venus kupoteza mfululizo kwa Serena.

Mwaka 2009 kwenye fainali za mashindano ya Wimbledon, – Serena alimzuia dada yake Venus kushinda taji la Tatu mfululizo la mashindano hayo baada ya kumnyuka katika mchezo huo na kutwaa taji la Tisa katika kipindi cha miaka Sita.

Mwaka 2017 kwenye fainali za Australian Open ambazo zilikuwa ni mara yao ya mwisho kukutana katika mashindano makubwa, Serena aliweka rekodi ya kushinda taji lake la 23 lenye hadhi ya grandslum na kutangaza kuwa wakati huo alikuwa na ujauzito wa miezi Mitatu.

Wanandugu hao kwa pamoja wamekusanya mataji 30 ya Grandslum katika mchezo wa tenisi tangu Venus aliposhinda mchezo wa hatua ya pili ya mashindano ya wazi ya Australia mwaka 1998.