Wachezaji wa Real Madrid wazoa tuzo

0
2738

Timu ya Real Madrid ya nchini Hispania ambayo ni mabingwa mara tatu mfululizo wa taji la ligi ya mabingwa Barani Ulaya baada ya kuinyuka Liverpool mabao Matatu kwa Moja katika fainali ya msimu uliopita, imefanya vizuri katika tuzo zote ambazo wachezaji wake waliwania.

Mlinda mlango wa timu hiyo Keylor Navas ameshinda tuzo ya kipa bora wa msimu, Sergio Ramos ametwaa tuzo ya beki bora huku Cristiano Ronaldo aliyehamia Juventus akishinda tuzo ya mshambuliaji bora wa msimu.

Katika tuzo hizo, nyota wa kimataifa wa Croatia, -Luka Modric ameshinda tuzo ya kiungo bora wa msimu pamoja na tuzo ya jumla ya mchezaji bora wa ulaya wa UEFA kwa msimu wa 2017/2018 baada ya kuwabwaga Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah.

Modric mbali na kushinda taji la ligi ya mabingwa Barani Ulaya na kikosi cha Real Madrid, aliisadia nchi yake ya Croatia kutinga fainali ya kombe la FIFA la dunia ambapo walipoteza mbele ya Ufaransa.

Nyota huyo amesema kuwa anajisikia furaha kushinda tuzo hizo na kwamba huu ni mwaka bora katika maisha yake ya soka kwa kuwa ndoto aliyoiota kwa muda mrefu tangu aanze kuichezea timu ya taifa imetimia.