Rais Magufuli aenda Afrika Kusini

0
505

Rais John Magufuli ameondoka nchini hii leo kwenda Afrika  Kusini ambapo kesho atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa.

Katika safari hiyo Rais Magufuli ameongozana na Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt  Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Philip Mangula na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa  Palamagamba Kabudi.

Wakizungumza kabla ya kuondoka nchini, Rais Mstaafu Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM Mangula wamesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na kwamba Serikali na chama zina kila sababu ya kudumisha uhusiano na ushirikiano huo.

Baada ya kuhudhuria sherehe hizo  za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Afrika Kusini, Rais Magufuli atafanya ziara rasmi ya Kitaifa nchini Namibia ambako pia atazindua mtaa uliopewa jina la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango mkubwa alioutoa katika ukombozi wa Taifa hilo.