Wasimamizi wa uchaguzi watakiwa kuzingatia sheria

0
496

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji  Mbarouk Salum Mbarouk amewataka  Wasimamizi wa uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria zinazosimamia uchaguzi nchini katika kusimamia uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 32 unaotarajiwa kufanyika Juni 15 mwaka huu.

Jaji Mbarouk ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa uchaguzi kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoka kata 32 na halmashauri 20 za Tanzania Bara zinazotarajia kushiriki katika uchaguzi huo.

Amesema kuwa pamoja na baadhi ya wasimamizi kuwa na uzoefu katika kusimamia chaguzi mbalimbali, ni vema wakazingatia maelekezo watakayopewa na Tume katika kusimamia uchaguzi huo badala ya kusimamia kwa mazoea kwani NEC imewaamini kuwa wanaweza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria.

“Ndugu washiriki mnatakiwa kutambua kuwa mmeaminiwa na kuteuliwa kwa sababu mnao uwezo wa kufanya kazi hii,  jambo la muhimu ni kujiamini na kujitambua na kwamba mtapaswa kuzingatia sheria, miongozo, kanuni na maelekezo yanayotolewa na Tume kwa ajili ya kuendesha na kusimamia chaguzi” amesema Jaji Mbarouk.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Dkt Athumani Kihamia amewataka wasimamizi hao wa uchaguzi kuwepo muda wote wakati wa kutekeleza majukumu ya uchaguzi na hata pale inapotokea dharura wahakikishe anakuwepo msimamizi atakayetekeza majukumu yao.

“Ni vyema mkafahamu kwamba kipindi hiki ambacho mmeshateuliwa na kuapa kuwa wasimamizi wa uchaguzi, wewe unakuwa mtumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa muda huo, kwa hiyo ni vema ukawa ofisini muda wote ukiondoa dharura” amesema Dkt Kihamia.