IFAD kufadhili miradi ya Shilingi Bilioni 127.3

0
388

Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umetenga Shilingi Bilioni 127.3 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kilimo nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2020.

Rais wa IFAD, – Gilbert Fossoun Houngbo amesema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Pamoja na kutenga fedha hizo, Houngbo ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Togo amempongeza Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza,  kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kukuza uchumi ikiwemo utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na IFAD, kutilia mkazo umuhimu wa uwekezaji usiokuwa tegemezi, unaolinda utu, unaozalisha kipato kwa wananchi na unaojenga misingi endelevu ya kujitegemea.

Amebainisha kuwa baada ya kutenga fedha hizo, IFAD inasubiri upande wa Tanzania kuainisha maeneo mahususi ya miradi ya kilimo ambako fedha zitaelekezwa na ameeleza kuwa ana matumaini miradi hiyo itafanikiwa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na namna Serikali ilivyo na dhamira ya maendeleo.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameushukuru Mfuko huo wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo kwa ushirikiano wake mzuri na Tanzania na amemhakikishia Houngbo kuwa ushirikiano huo ulioanza mwaka 1978 utadumishwa kwa maslahi ya Watanzania.

Rais Magufuli ameongeza kuwa fedha zilizotengwa katika mpango huo wa miaka mitatu zitaelekezwa katika maeneo yenye maslahi mapana ya sekta ya kilimo ikiwemo kuwezesha matumizi ya zana bora za kilimo katika uzalishaji, kuzalisha mbegu bora za mazao, kutatua changamoto ya masoko ya mazao, kuboresha ufugaji na ameipongeza IFAD kwa kutoa fedha pasipo kuweka masharti ya maeneo zinakopaswa kuelekezwa.

Kufuatia ufadhili huo, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kuharakisha mchakato wa kuainisha maeneo yatakayopokea fedha hizo ili utekelezaji wa mpango huo uanze.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden, – Peter Eriksson.

Baada ya mazungumzo hayo, Eriksson amempongeza Rais Magufuli na Serikali yake kwa mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ameeleza dhamira ya Sweden kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjöberg na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Profesa  Palamagamba Kabudi.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemuapisha Dkt Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Hafla ya kuapishwa kwa Balozi Ulisubisya imefanyika Ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.