Sevilla kuwasili nchini kesho

0
385

Miamba ya soka katika ligi soka daraja la kwanza nchini Hispania-Maarufu La Liga, Timu ya Sevilla inatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya Simba, mchezo utakaochezwa Alhamisi Mei 23 mwaka huu katika  uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Ziara ya Sevilla hapa nchini itahusisha pia matukio kadhaa ya kijamii na michezo,  ikiwemo kliniki na mafunzo mbalimbali.

Ujio wa timu hiyo ni kwa udhamini wa Sportpesa ikiwa ni sehemu ya mradi wa La Liga duniani unaolenga kueneza soka la Hispania Kimataifa na kueneza pia sera ya Marca Espana ambayo ni kuleta karibu mashabiki wa La Liga na kukuza klabu nje ya nchi yao.

Sevilla juzi Jumamosi walipata ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi ya Athletic Bilbao katika mchezo wao wa mwisho wa La Liga kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Ramon Sanchez Pijuan na kumaliza ligi hiyo wakiwa na alama 59 na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Yuropa League msimu ujao, michuano wanayoionea mara nyingi wakiwa wameshabeba taji lake mara Tano.

Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki kati ya Simba dhidi ya Sevilla, utatangazwa Mubashara na TBC Taifa na kuonyeshwa pia mubashara kupitia Chaneli ya Utalii ya TBC 3 ambayo ni Tanzania Safari Channel.