Kagere aelezea mchezo wa Simba na Wanakuchere

0
364

Mshambuliaji wa timu ya Simba, – Meddie Kagere amesema kuwa licha ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao Mawili kwa bila dhidi ya Wanakuchere Ndanda FC, mchezo huo ulikuwa mgumu kwao na walilitarajia hilo.

Kagere ambaye mabao yake mawili aliyofunga hapo jana yamempa ukinara katika ligi hiyo akizidi kupaa na mabao yake 22,  sasa anasema wanashukuru kupata ushindi huo na sasa wanaelekeza nguvu katika michezo mitatu iliyosalia ukiwemo ule wa kesho dhidi ya Singida United katika dimba la Namfua mkoani Singida.

Simba wanasaka alama moja tu ili kujihakikishia kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu,  wakiwa tayari na alama zao 88 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku wakiwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga, wakiwa wamefunga mabao 74 ikiwa ni mabao 19 zaidi ya mabao ya mahasimu wao Yanga wenye mabao 55.

Simba pia wanafaida ya wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa wakiwa wamefungwa mabao machache zaidi, mabao 14 ambapo ukiyatoa katika mabao yao 74 waliyofunga, wanakuwa na wastani wa mabao 60, hii ni tofauti ya mabao 30 dhidi ya yanga.

Naye kocha Mkuu wa timu ya Yanga, – Mwinyi Zahera bado hajakata tamaa ya Ubingwa,  na kwa sasa anasema nguvu na akili yake ameielekeza kwenye maandalizi ya michezo ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili waweze kupata matokeo chanya .

Yanga watacheza na Mbeya City siku ya Jumatano katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, kisha watamalizia na Azam FC Mei 28 mwaka huu katika uwanja huo huo wa Uhuru.

Yanga wakishinda michezo yote hiyo miwili,  watafikisha alama 89 ambazo Simba wakipata sare tu katika mchezo wao wa kesho dhidi ya Singida United watakuwa wameshazifikia na kuwa na uhakika wa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.