Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuondoa adha ya kukosekana kwa vifaranga vya kuku bora nchini pamoja na tatizo la upatikanaji wa chakula bora cha kuku.
Waziri Mkuu Mstaafu Pinda ambaye pia ni mlezi wa Chama Cha Wafugaji Kuku Bora mkoani Dodoma (CHAWAKUBODO) ametoa ombi hilo jijini Dodoma wakati chama hicho kikipokea msaada wa vifaranga vya kuku bora kutoka Kampuni AKM Glitters.
Amesema kuwa ukosefu wa vifaranga na chakula bora cha kuku unasababisha wafugaji wengi kukosa ari ya kuendelea kufuga.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amekiri kuwepo kwa tatizo la upatikanaji wa chakula bora cha kuku nchini na kusema kuwa suala hilo ni lazima lishughulikiwe kuwaondolea kero wafugaji.
Ameongeza kuwa kukosekana kwa vifaranga bora nchini kumetokana na udhibiti wa uingizwaji holela wa vifaranga vya kuku na kwamba kwa sasa tatizo hilo lipo katika hatua za utatuzi ili hali ya upatikanaji wa vifaranga irejee kama zamani.
“Tumekubaliana lazima kuwe na udhibiti wa utotoleshaji wa vifaranga kiholela na utengenezaji wa vyakula vya mifugo jambo litakalosaidia kuondoa tatizo la kuwa na vifaranga na vyakula visivyo na ubora” amesema Naibu Waziri Ulega.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Patrobas Katambi amewapongeza wafugaji hao na kusema kuwa kwa sasa sekta ya ufugaji inakua hivyo ni lazima changamoto zilizopo zitatuliwe.
Chama cha Ushirika wa Wafugaji Kuku mkoa wa Dodoma kimepokea msaada wa vifaranga Elfu Nne ikiwa ni awamu ya kwanza ya msaada huo.