Raptors watinga fainali NBA Kanda ya Mashariki

0
360

Toronto Raptors wametinga fainali ya Mashindano ya Mpira wa Kikapu wa Kulipwa nchini Marekani ( NBA) kwa Kanda ya Mashariki baada ya kuilaza Philadelphia 76’ERS alama 92 kwa 90 katika mchezo wa Saba wa hatua ya nusu fainali uliopigwa kwenye dimba la Scotia Bank mjini Toronto huko Canada.

Kahwi Leornard ameibuka shujaa wa Raptors akiwapeleka fainali kwa kufunga alama mbili muhimu katika sekunde ya mwisho ya mchezo zilizomfanya kufunga jumla ya alama 41 katika mchezo huo huku akicheza mipira iliyorudi yaani Rebounds Nane huku Serge Ibaka akifunga alama nyingine 17.

Licha ya Joe Embiid kufunga alama 21 na kucheza Rebounds 11,  bado hazikutosha kuipa Sixers ushindi wa ugenini katika mchezo huo wa Saba ulioamua timu ya kwenda fainali baada ya kutoka sare ya michezo Mitatu Mitatu katika michezo Sita iliyopita.

Kwa ushindi huo,  Toronto Raptors sasa watamenyana na Milwaukee Bucks katika fainali ya Kanda ya Mashariki ambapo Bucks walitangulia kutinga fainali kwa kuwashinda Boston Celtics kwa michezo Minne kwa Mmoja katika nusu fainali. 

Kwenye kanda ya Magharibi, – Portland Trail Blazers nao wametinga fainali baada ya kushinda mchezo wa Saba wa nusu fainali dhidi ya Denver Nuggets kwa alama 100 kwa 96.

CJ Mc Colum amefunga alama 37 na kucheza Rebounds  Tisa huku Damian Lillard akifunga nyingine 17 na kuivusha Blazzers katika fainali ambapo watamenyana na bingwa mtetezi wa NBA, Golden State Warriors kutafuta mbabe wa Kanda ya Magharibi.