Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji amesema kuwa serikali ya Tanzania na serikali ya Cyprus zimekubaliana kuwalipa wateja wa Benki ya FBME baada ya serikali ya Tanzania kuamua kuifilisi benki hiyo.
Akijibu swali Bungeni jijini Dodoma, Dkt Kijaji amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006, wateja wanaoweka fedha zao ndani ya benki au taasisi za fedha ni lazima walipwe amana zao, pindi benki ama taasisi husika ya fedha itakapofilisiwa.
Dkt Kijaji amewataka wateja ambao wameweka amana zao zaidi ya Shilingi Milioni Moja na Nusu katika benki hiyo ya FBME kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha amana hizo zinalipwa .
Pia amewaondoa hofu Watanzania wote kuwa Benki zilizopo nchini na taasisi nyingine za Kifedha ziko salama, hivyo hawana sababu ya kuwa na hofu ya kuweka fedha zao benki.
Bunge linaendelea na mkutano wake wa 15 jijini Dodoma ambapo Wabunge wanaendelea kujadili bajeti za wizara mbalimbali kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
