Benki ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa dola Bilioni 1.46 za Kimarekani ambazo ni sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 3.3 kwa ajili ya kujenga kipande cha reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kuanzia Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mtendaji wa Benki hiyo Bill Winters.
Dkt Mpango ameishukuru benki hiyo kwa kukubali kugharamia ujenzi wa reli hiyo ya kisasa ambayo lengo lake ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwenda bara na nchi jirani za Maziwa Makuu na zile ambazo hazipakani na Bahari.
“Tunajenga reli hiyo ya Kisasa kutoka Dar es salaam – Morogoro hadi Makutupora ambazo ni awamu mbili lakini pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa nchi ya Rwanda, tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali” ameongeza Dkt Mpango
Waziri huyo wa Fedha na Mipango amemueleza mkurugenzi mtendaji huyo wa Benki ya Standard Chartered Group Bill Winters anayeongoza benki hiyo kwenye nchi zaidi ya Sitini duniani kuhusu vipaumbele vikubwa vya Tanzania ambavyo ni pamoja na kuboresha Kampuni ya Ndege Nchini (ATCL) na Ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa Mto Rufiji.
Kwa upande wake Winters ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na kwamba Benki ya Standard Chartered Group itatoa mkopo nafuu wa dola Bilioni 1.46 za Kimarekani kwa Tanzania na kuahidi kuwa balozi wa kuelezea mafanikio makubwa ya kiuchumi ya Tanzania kwa wadau wengine.
Pia ameahidi kuzishawishi taasisi nyingine za fedha ulimwenguni kuangalia uwezekano wa kuunga mkono jitihada hizo ambazo mwisho wake wanufaika wakubwa watakuwa ni wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.