Baada ya ushindi dhidi ya Barcelona ya Hispania, Kocha wa Klabu ya Liverpool ya nchini England, – Jurgen Klopp amewapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kupindua meza kibabe katika mchezo wa marejeano wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya hatua ya nusu fainali.
Majogoo hao wa Anfield, – Liverpool walishinda kwa magoli manne kwa bila na kulipa kisasi cha kupigwa mweleka wa magoli matatu kwa bila walipocheza ugenini Nou Camp wiki iliyopita, hivyo kutinga Fainali kwa jumla ya magoli manne kwa matatu.
Magoli ya Liverpool yamefungwa na Divock Origi na Georginio Wijnaldum ambao walifunga mawili kila mmoja.
Liverpool imetangulia fainali na kusubiri mshindi wa jumla baina ya Tottenham ya England na Ajax Amsterdam ya Uholanzi, mchezo utakaopigwa usiku wa leo.
Katika mchezo wa awali ambao Ajax walikuwa ugenini huko nchini England, waliifunga timu ya Totternham Hospur goli moja kwa bila, hivyo Totternham inahitaji nayo kupindua matokeo ili iweze kutinga fainali.
Baadhi ya mashabiki wa Liverpool wameufananisha ushindi huo na ule wa mwaka 2005 ambapo Liverpool ilitoka nyuma kwa magoli matatu kwa bila dhidi ya AC Milan hadi kipindi cha nusu ya kwanza lakini kipindi cha pili ikayarejesha yote na kutwaa taji la UEFA kwa mikwaju ya penati.
