Iran kuongeza urutubishaji wa madini ya Uranium

0
435

Iran imesema kuwa itaongeza urutubishaji wa madini ya uranium baada ya siku Sitini, ikiwa ni mwaka mmoja toka Marekani ijiondoe kwenye mkataba wa Kimataifa unaolenga kukabiliana na utengenezaji wa nyuklia.

Rais Hassan Rouhani wa Iran  amesema kuwa baada ya siku hizo Sitini,  Iran itaongeza zaidi urutubishaji wa madini hayo ya uranium yanayotengeneza nyuklia ambayo yamezuiwa kwenye mkataba huo.

Mkataba huo wa Kimataifa unalenga kukabiliana na utengenezaji wa nyuklia nchini Iran, ili nchi hiyo iweze kuondolewa vikwazo vya misaada.

Mkataba huo ulikubaliwa na Iran na mataifa mengine Wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Russia na Ujerumani na uliingia dosari  baada ya Rais Donald  Trump  wa Marekani kutangaza kujiondoa mwaka mmoja uliopita.

Tangu wakati huo,  thamani ya fedha ya Iran ilishuka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, mfuko wa bei uliongezeka na Wawekezaji wa kigeni waliondoka nchini humo.