Federer afanya kweli

0
2313

Bingwa mara Tano wa michuano ya wazi ya Tenisi ya Marekani, – Roger Federer wa Uswisi ametinga hatua ya mzunguko wa pili katika michuano hiyo baada ya kupata ushindi wa seti tatu kwa bila dhidi ya Yoshihito Nishioka wa Japan.

Federer amemnyuka Nishioka kwa matokeo ya 6-2, 6-2 na 6-4 na kusonga mbele akitumia muda wa saa moja na dakika 52.

Federer ambaye ni mshindi wa mataji 20 makubwa ya Tenisi yaani Grand Slam atacheza na Benoit Paire wa Ufaransa katika mzunguko wa pili wa mashindano hayo.

Naye Novak Djokovich wa Serbia amefanya kweli na kufanikiwa kutinga hatua ya pili kwa kupata ushindi wa seti tatu kwa moja dhidi ya Marton Fucsovich wa Hungary.

Djokovich amepata ushindi huo katika seti nne kwa matokeo ya 6-3, 3-6, 6-4 na 6-0 ambapo mchezo huo ulilazimika kusimamishwa kwa dakika kumi ili kutoa nafasi kwa wachezaji kupoza joto kwa kupata maji.

Djokovich ambaye ni bingwa wa michuano hiyo mwaka 2011 na 2015, sasa atachuana na Tennys Sandgren wa Marekani katika hatua ya pili ya mashindano hayo.

Kwa upande wa kinadada, baada ya Serena Williams kuanza vyema na kuwasha moto wa ushindi mbele ya Magda Linette, mchezaji namba moja kwa ubora wa tenisi nchini England, Yohana Conta ametupwa nje ya mashindano hayo kutokana na kula mweleka wa seti mbili kwa bila dhidi ya Caroline Garcia.
Conta amenyukwa 6-2 na 6-2 huku pia bingwa mtetezi kwa kinadada Sloane Stephens wa Marekani akianza vyema kampeni yake kwa kupata ushindi dhidi ya Evgeniya Rodina.