Waziri Mkuu asisitiza uadilifu

0
2335

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ukosefu wa uadilifu ni moja ya eneo ambalo lilitia doa utendaji wa sekta binafsi hususan pale ambapo ilishirikiana na serikali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam wakati akifungua mkutano mkuu wa 18 wa mwaka wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania –TPSF, kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Waziri Mkuu amesema uadilifu ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na serikali na TPSF.

Pia Waziri Mkuu ameitaka TPSF ijifunze kwa walioendelea kwa kutokuwa na vitendo vya rushwa na kutoa adhabu kwa wanaoenda kinyume na misingi ya uadilifu waliojiwekea.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kuboresha miundombinu, kutoa vivutio kwenye kodi, kanuni na sheria ili kukuza sekta binafsi.

Amewasihi TPSF kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa bidhaa za viwandani na wahakikishe kuwa wanajali maisha ya Watanzania ambao ndio soko na wateja wa bidhaa zao.