Wawrinka ambwaga Dimitrov

0
2239

Nyota wa mchezo wa tenisi Stan Wawrinka amembwaga Grigor Dimitrov katika mzunguko wa kwanza wa mashindano ya wazi ya Marekani kwenye uwanja wa Flushing Meadows jijini New York.

Hii ni mara ya pili mfululizo ambapo Wawrinka anamtoa Dimitrov kwenye michuano mikubwa katika hatua za awali ambapo katika mzunguko huo amemfunga seti tatu kwa bila za 6-3, 6-2 na 7-5.

Nyota huyo raia wa Switzerland alikosa michuano ya mwaka 2017 kutokana na kuuguza majeraha ya goti alilofanyiwa upasuaji mara mbili na kumfanya ashindwe kutetea taji alilotwaa mwaka 2016.

Katika matokeo mengine Andy Murray ameanza vyema mashindano hayo mara baada ya kumfunga James Duckworth wa Australia seti tatu kwa moja za 5-7, 6-3, 7-5 na 6-3 kwenye uwanja wa Louis Armstrong.

Murray atakutana na mkongwe Fernando Verdasco wa Hispania katika mchezo wa hatua ya pili.