Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikifanikiwa katika kampeni zake mbalimbali za hamasa kwa jamii kutokana na nguvu pamoja na sauti ya Viongozi wa dini.
Waziri Mkuu amesema hayo katika Baraza la Maulid lililofanyika kitaifa mkoani Dodoma ambapo amesema hiyo ni kutokana na Viongozi wa dini kutimiza majukumu yao katika mafundisho ya kiroho kwa Waumini wao na hivyo imewarahishia Viongozi wa Serikali kutimizia majukumu yao kwa weledi katika kuleta maendeleo.
“Suala ambalo ningependa kusisitiza ni ushiriki wa madhehebu ya dini katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwani kwa sasa limekuwa tatizo kubwa na hasa matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya Duniani limekuwa kubwa, na Taifa letu pia linapitiwa na wimbi hili”. amesema Waziri Mkuu.
Amesema zamani ilizoeleka matumizi ya dawa za kulevya ni mijini lakini kwa sasa matumizi ya dawa za kulevya yanawafikia hadi Wananchi wa vijijini hasa vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa.
“Lakini pia hata baadhi ya watoto wetu wapo hatarini zaidi katika kutumbukia kwenye janga hili kutokana na ushawishi wa rika na uwezo mdogo katika maamuzi yao”. ameongeza Waziri Mkuu.
Amewasihi Viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kukabiliana na matatizo ya kupoteza nguvu kazi.