Dkt. Mollel : Huduma za Maabara ni msingi wa Hospitali

0
117

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Huduma za maabara ndiyo msingi mkuu wa Hospitali katika kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.

Dkt. Mollel amebainisha hayo mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mkutano wa mwaka wa 36 wa Chama cha wataalamu wa maabara nchini ambapo amesema kuwa kiasi cha Shilingi trilioni 6.7 kilichowekezwa kwenye sekta ya afya nchini asilimia kubwa imelenga kwenda kuboresha Huduma za maabara.

Dkt. Mollel amesema jiwe la msingi katika sekta ya afya ni maabara hivyo serikali itaendelea kuboresha Huduma za maabara katika hospitali zote nchini ili wananchi waweze kupata Huduma bora.

“Hospitali yoyote msingi wake ni maabara ndiyo maana mtaona hivi sasa serikali yetu ya awamu ya sita chini ya uongozi imara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuwekeza kwenye Huduma za maabara kwa kufunga mashine za MRI, CT Scan na mashine nyine za kupima vimelea vya magonjwa mbalimbali katika hospitali zote nchini”- ameeleza Dkt. Mollel

Amesema maabara ni muhimu sana kwani zimekuwa msaada wakati inapotekea mlipuko wa magonjwa mbalimbali na kusaidia kutambua sambuli kwa wakati.

“Tulipambana na UVIKO-19 watu wa maabara ndiyo walikuwa msaada lakini pia tulipambana na homa ya mgunda watu waliokuwa mstari wa mbele ni wataalam wa Huduma za maabara”- amesisitiza Dkt. Mollel

Aidha amesema lengo la kongamano hilo ni wataalam wa Huduma za maabara nchini kukaa na kujadili kwa namna gani wataboresha huduma hizo ngazi ya taifa hadi ngazi ya msingi.