Mfumo wa kielektroniki unaowezesha kufanya usajili, kuchakata zabuni, kusimamia mikataba, malipo na kununua kupitia katalogi na minada kimtandao (NeST) uliotengenezwa na Watanzania unatarajiwa kudhibiti vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kughubika michakato wa ununuzi Serikalini.
Uhakika huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania na kuongeza kuwa mfumo huo wa kisasa utarahisisha zaidi michakato ya manunuzi.
Akieleza ufanisi wa mfumo huo, amesema awali katika mfumo wa TANePS walilazimika kufanyia michakato yote pembeni kisha kuipakia (upload) taarifa kwenye mfumo, lakini kupitia NeST, michakato itafanyika kwenye mtandao na hivyo kutoa uwazi kwa wazabuni na umma kuona mwenendo mzima.
Aidha, mfumo huo utaondoa malalamiko ya watu kukosa tenda kwa sababu utaonesha sababu za mwombaji kukosa, pia utaongeza ushindani kwa kuonesha idadi ya tenda zilizopo, tenda zilizoombwa, tenda zilizo wazi, utaonesha ni nani anayechelewesha mchakato kukamilika pamoja na taarifa nyingine muhimu katika manunuzi.
“Ule mfumo tunaoachana nao, kampuni moja ya Kigiriki ilituuzia. Lakini kama Taifa, mkitengeneza mfumo wenu, maana yake taarifa zote na takwimu zote mnazo nyie wenyewe. Lakini ule mwingine, hata Mgiriki yule alikuwa anaona tunachofanya. Sasa hivi tunaona sisi wenyewe,” amesema Maswi akieleza namna mfumo mpya unavyotekeleza sera ya usiri wa taarifa.
Amesema mfumo huo utaanza kutumika rasmi Septemba 30 mwaka huu ambapo NeST utatumika kwenye taasisi zote na kwamba kwa mujibu wa sheria mpya Afisa Masuuli asipotumia mfumo ataweza kutozwa faini isiyopungua milioni 10, kifungu kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.