Mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la Colletha Francis, Mkazi wa kijiji cha Ihunga wilayani Muleba mkoani Kagera ameuawa kwa kuchomwa moto akiwa ndani ya nyumba yake na watu wasiojulikana.
Chanzo cha mauaji hayo kinaelezwa ni kupotea kwa mtoto Ismail Khamis toka Aprili Tano mwaka huu na mwili wake kukutwa umezikwa shambani kwa mwanamke huyo.
Imeelezwa kuwa mwili wa mtoto huyo uligundulika umezikwa katika shamba la Marehemu Colletha ukiwa wima, baada ya mbwa aliyekuwa akipita maeneo hayo kufukua sehemu hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Muleba, -Richard Ruyango amefika katika kijiji hicho cha Ihunga na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi huku akiwataka viongozi wa dini kuingilia kati suala hilo kwa kuzikutanisha familia mbili zilizokumbwa na vifo hivyo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kagera, – Revocatus Malimi amethibitisha kutokea kwa kifo cha Colletha na kupatikana kwa mwili wa mtoto huyo.