Mavunde atangaza vita na watorosha madini

0
124

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa ataweka mkazo mkubwa katika kudhibiti vitendo vya utoroshaji madini, ikiwa ni moja ya mikakati yake ya kukuza sekta hiyo, ili kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu inauzwa katika mfumo rasmi ili iweze kuwanufaisha Watanzania wote.

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC, Mavunde amesema sekta ya madini imeendelea kuonesha mwelekeo chanya, ikiwemo mchango wake kwenye uchumi, hivyo wamejipanga kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Mbali na kudhibiti utoroshaji madini, amesema mkakati mwingine wanaouchukua kuongeza tija ni kuimarisha masoko na vituo vya kuuza madini ambayo yataongeza makusanyo ya sekta hiyo kufikia lengo la shilingi trilioni 1 katika mwaka 2023/24.

Aidha, amesema wachimbaji wadogo wana mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta hiyo, akitolea mfano kuwa katika maduhuli ya shilingi bilioni 648 yaliyokusanywa mwaka 2022/23, zaidi ya asilimia 40 zilitoka kwa wachimbaji wadogo. Kutokana na mchango wao mkubwa, Serikali itaendelea kuwawezesha wafanye kazi zao kwa ufanisi zaidi, ambapo moja ya hatua inayochukuliwa ni kusajili wachimbaji wote nchini, ili kuwa na taarifa zao ikiwemo eneo walipo na shughuli wanayofanya.

Katika mwaka uliopita sekta hiyo ilichangia asilimia 15 ya makusanyo yote, asilimia 56 ya fedha za kigeni na ilikuwa na mchango wa asilimia 9.1 kwenye pato la Taifa ambapo lengo ni kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.