Mtoto wa Tembo aokolewa kutoka shimoni

0
141

Askari wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamefanikiwa kuokoa mtoto wa tembo mwenye umri wa takribani wiki nne aliyekuwa amezama katika shimo lenye matope katika Kijiji cha Kwamsanja, kilichopo kata ya Kibindu, Halmashauri ya Chalinze, karibu na Pori la Akiba la Wamimbiki.

Taarifa za mtoto huyo wa tembo aliyetelekezwa na kundi lake na kuangukia shimoni zilitolewa na raia mwema aitwaye Manase Thomas Baha, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kwamsanja. Taarifa hizo zilimfanya Kamanda wa Pori la Akiba la Wamimbiki, Emmanuel Lalashe, kutuma timu ya askari wanne (4) kushirikiana na askari wa Jeshi la Akiba (migambo) sita (6) kwa ajili ya zoezi zima la kuokoa mtoto huyo wa tembo.

Akizungumza baada ya zoezi la uokoaji, Kamanda Lalashe aliwashukuru wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Wamimbiki kwa ushirikiano wao katika kulinda rasilimali za nchi, hasa rasilimali za wanyamapori katika hifadhi hiyo. Rasilimali hizi za wanyamapori ni muhimu kwa shughuli za utalii na pato la taifa.